Saturday, May 9, 2009

Mwakyembe: haikuwa rahisi kuipa chati TBS

Na Sarah Mossi
Rai; Alhamis 15-21, Mei 2008

§ Ni maabara ya kwanza Tanzania Kujulikana kimataifa
§ Hata baada ya kustaafu amebaki kuwa kama chapa yake
§ Ni mtaalamu wa viwango, na alivisimamia mwenyewe
§ Sasa aanzisha TCAS kutetea haki na sauti za walaji wote

Leo hii ukiyaangalia mafanikio ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS), hukosi kumhusisha na maendeleo hayo aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu, Daimon Mwakyembe, ambaye sasa amestaafu.

Mwakyembe (61) amestaafu lakini atabaki kuwa ni kielelezo kizuri cha mafanikio yaliyopatikana ndani ya shirika hili kongwe nchini, alisukuma vyema maabara, alijituma na kubuni mikakati mbalimbali kuhakikisha TBS inakuja juu.

Huyu ni mmoja wa wale wazee waliotumikia taifa hili miaka mingi, tena kwa uaminifu, hii ni hazina ya taifa kwa maneno mengine. Ukiitaja TBS leo hii kwenye kundi la watu, wengine watakuuliza ni ile ya Mwakyembe? Wakimaanisha kwamba iliyokuwa inaongozwa na mwakyembe. Kumbe basi tunaweza kusema lwamba Mwakyembe ni sawa na chapa ya TBS.

Kutokana na umuhimu wake kwa Taifa hili, baada ya kustaafu mwaka 2006, Rai ilimtafuta Mwakyembe kwa mahojiano maalumu, hata hivyo aliomba aachwe kwa wakati huo apumzike. Mwakyembe alikataa kufanya mahojiano wakati huo kwa kigezo kuwa asije kuonekana ‘kimbelembele’au kwamba alikuwa anataka umaarufu. Bahati nzuri tulimuelewa.

Baada ya kipindi kirefu cha ukimya, Rai ilimtafuta tena mwakyembe na kumsihi akubali kufanya mahojiano, akakubali na Mei 7 mwaka huu alifanya hivyo kwa lengo la kuielezea jamii anafanya nini sasa baada ya kulitumikia Taifa miaka mingi kiasi hicho.

“Nilijiunga na TBS mwaka 1979, nikitokea TIPER ambapo nilifanya kazi kwa miaka saba, kule ndiko nilikojifunzia mambo ya viwango.”

Hii ndiyo kauli aliyoanza nayo Mwakyembe katika mahojiano yetu, akieleza namna alivyopata ujuzi wa kuelewa masuala ya viwango vya bidhaa. Anasema kwamba alipojiunga TBS, moja kwa moja akafanya kazi ndani ya maabara, akiwa na mtaalamu wa kuangalia viwango vya petrol na gesi mbalimbali, kama oksijeni, naitrojeni na kaboni dayoksaidi.

Mwakyembe anasema kwamba alifanya kazi hiyo kwa muda na baada ya kutangazwa nafasi za utawala, akapandishwa cheo na kuwa meneja viwango. Aidha anasema mwaka 1992 walistaafu wakurugenzi wengi ndani ya TBS, akiwamo aliyekuwa Mkurugenzi mkuu, Benedict Mwobahe, hapa ndipo alipokabidhiwa jukumu la kuliendesha shirika hilo.

“Unajua mimi nilitoka kiwandani, nilijua kusukuma maabara za TBS na viwango navielewa, kuna International Accreditation, hii nidyo najivunia, nimeandika viwango na kusimamia maabara mwenyewe, TBS ni maabara ya kwanza Tanzania kujulikana kimataifa na kupata sifa, hili nimesimamia mwenyewe.

“Kabla ilikuwa haijulikani kimataifa, lakini sasa viwango vya TBS vinajulikana kimataifa kama kwenye vyakula, bidhaa hata kwenye minofu ya samaki.

Anasema viwango vya TBS vilianza kujulikana kimataifa, Novemba 1996 na kusisitiza sheria za kimataifa za viwango zinasema ili maabara ijulikane kimataifa ni lazima watalamu wa kimataifa waangalie hali ya maabara, ujuzi wa wataalamu, kemikali zinazotumika, pamoja na vyombo vinavyotumika kama vinakubalika kimataifa.

“Sisi kwetu walikuja wataalmu kutoka South Africa National Accreditation System, waliangalia ujuzi wetu, wataalamu, hali ya maabara yetu, vyombo vianavyotumika na kemikali, wakaafiki na kutuma cheti cha kiamataifa,” anasema Mwakyembe.

Lakini anaongeza kwamba, kazi ya kulifikisha shirika hilo hapo lilipo na viwango vyake kujulikana kimataifa haikuwa rahisi kama wanavyodhani, hasa baada ya kukabidhiwa kuliongoza mwaka 1992.

Anasema alipewa kazi ya kuongoza shirika hilo huku likiwa likikabiliwa na ukapa mkubwa wa fedha za kujiendesha. Anasema serikali wakati huo ilikuwa haitoi fedha za kuendesha maabara.

Hata hivyo, anabainisha kwamba hakukata tama, hivyo alianza kubuni mikakati ya kutafuta fedha za kujiendesha, akafanikiwa kukopa Sh milioni 15 kutoka mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Anasema kwamba fedha hizo zilitumika kujenga baadhi ya majengo ya utawala, lakini kutokana na uhaba wa fedha wakashindwa kurejesha mkopo huo na NSSF wakakamata gari na vifaa vyote vya shirika.

Kwa mujibu wa Mwakyembe, tatizo lingine alilokumbana nalo alipoteuliwa kuwa Mkurugenzi mkuu ni kutokaguliwa ipasavyo hesabu za TBS. Anasema kipindi hicho ajira pia zilisimama.

Aidha, anasema kwamba kutokana n akuwa na uongozi wa pamoja ndani ya shirika hilo, waliweza kubuni mikakati ya kurejesha fedha hizo na kufanikiwa kulipa deni pamoja na kununua magari ya ofisi pamoja na vifaa vya ofisi.

“Miaka mitano ya mwanzo, mara baada ya kukabidhiwa shirika ilikuwa ni migumu kwangu lakini baada ya miaka 10 tutaweza kujikwamua na sasa wananchi wanajua 0.
umuhimu wa viwango, sasa maabara inatambuliwa kimataifa, TBS inatambuliwa na wananchi, hesabu za TBS zilikuwa hazikaguliwi ipasavyo, lakini baada ya miaka 10 hadi naondoka hesabu zinakwenda vizuri,”anasisistiza.

Mwakyembe anasema kwamba wakatai akiwa madarakani ya kuajiri na kutoa mafunzo kwa vijana wapya kwa kuamini kuwa wakati atakapostaafu bila shaka angefuatiwa na wengine ambao walitakiwa kustaafu kwa mujibu wa sheria na hiyo ingewapa wakati mgumu kutafuta watu wa kushika nafasi zao.

Mwanzoni tuliacha kuajiri, lakini nikaona mara nitakostaafu ningefuatiwa na wengine 10 waliotakiwa kustaafu, tukaanza kuajiri vijana ili tukiondoka wachukue nafasi zetu.

Mwakyembe anajivunia uongozi wa pamoja uliokuwapo ndani ya TBS, wakati akiwa mkurugenzi mkuu a hiyo anasema ilikuwa ni furaha yake kubwa.

“Sikumbuki kuchukua uamuzipekee bila kushirikisha mameneja au wafanyakazi, kama ni makosatulifanya wote, tulifanya kitu kwa uwazi na uongozi wa pamoja. Tumeweza kuboresha maslahi ya wafanyakazi, kuongeza marupurupu, tuliamini wafanyakazi wakilipwa vizuri wataweza kuepuka rushwa, najivunia mno kuboresha maslahi ya wafanyakazi,”anasema.

Mwakyembe pia anajivunia kurejesha uhusiano uliovunjika kati ya Jumuiya ya Wafanyakazi wa TBS na menejimenti, ambao ulizua migogoro ya mara kwa mara kwenye shirika.

“Nakumbuka wakati nachukua shirika mwaka 1992, kulikuwa na uhasama mkubwa kati ya wafanyakazi na menejimenti, nikayamaliza kwa pamoja na sasa uhusiano kati ya menejimenti na jumuiya yao umerudi.”

Mwakyembe anashukuru bodi ya Wakurugenzi ya TBS pamoja na aliyekuwa waziri wa viwanda na biashara wakati huo, Cleopa Msuya kwa kumuunga mkono wakati wote akiwa mkurugenzi mkuu na kusimama kidete kuhakikisha shirika linapata wafadhili mbalimbali kuweza kujiendesha, tofauti na miaka ya nyuma.

“Nazishukuru bodi tatu za mwisho zilitusapoti na kwa kutumia bodi hizi shirika sasa linakwenda vizuri, tukapata wafadhili, David Cleopa Msuya alipokuwa waziri wa Viwanda alitafuta wafadhili SIDA ambao wamejenga yale majengo, kupitia Bodi, serikali ilitusaidia. Lakini nawashukuru mawaziri wote baadae kwa ujumla walitusaidia,” anasisitiza.

Wahenga walisema ujuzi hauzeeki, msemo huo Mwakyembe anautumia ipasavyo na anasema kuwa bado anaendeleza taaluma yake na hayupo mbali na alichokuwa akifanya TBS. Anasema mwanadamu anaweza kuzeeka lakini ujuzi hauzeeki na sasa ameamua kuanzisha Sharika binafsi la kujitolea litakalokuwa na jukumu la kumlinda mlaji (mtumiaji wa bidhaa nchini). Analitaja shirika lenyewe kwamba litajulikana kama Shirika la kutetea Haki za Mlaji Tanzania (TCAS).

Anafafanua kwa kusema kuwa katika utengenezaji bidhaa, kunahitajika mambo matatu ambayo ni mzalishaji, viwango na mlaji.

Anasema katika nchi zilizoendelea kama Marekani, Uingereza, mlaji au mtumiaji wa bidhaa ana sauti katika viwango na kupima. Anasema kwa Tanzania mambo ni kinyume kwa mtengenezaji kuwa na sauti dhidi ya mlaji.

Anaongeza kwamba hali hiyo imemsukuma kuanzisha shirika hilo litakalokuwa na jukumu la kutetea haki za mlaji pamoja na kuyafanya matakwa yake kufanyiwa kazi na watengenezaji bidhaa.

“Hapa kwetu mlaji anamtegemea TBS tu, hajui haki zake na hii tunataka Tanzania mlaji ajue haki zake, nimeanzisha shirika hili mwaka jana, nipo na wenzangu, ndio kwanza tunatafuta wafadhili,”anasema.

Hakuna ubishi kwamba kazi nyingi za TBS kabla zilikuwa hazijulikani na ilifikia wakati wananchi wakawa na maswali mengi yasiyo na majibu juu ya utendaji wa kazi wa shirika hilo.

Mwakyembe katika hilo anakiri na kusema hali hiyo ilitokana na shughuli nyingi za shirika kufanywa kimya kimya na pengine kinyemela zaidi. Anasema mara baada ya kukabidhiwa shirika alipata kuhudhuria moja ya kozi zilizoendeshwa na Taasisi ya Menejimenti ya Ireland, katika programu ya maofisa wakuu wa mashirika kwa ajili ya kuwezesha kuendesha mashirika yao.

“Ilikuwa nzuri, katika programu moja ya marketing (masoko) Mwalimu akasema lazima kila siku ufanye ubunifu, uunde na usherehekee, sasa nikasema kumbe ni lazima usherehekee. Hivi vyeti vya ubora wa bidhaa tulikuwa tunatoa kinyemela, niliporudi nikasema, kumbe lazima hivi vyeti tuvitoe kwenye sherehe na watu wakutusaidia ni media (vyombo vya habari).

“Nikasema bila Media huwezi ku celebrate na wananchi wakakusikia, nikasema Media wakijua watatutangaza nchi nzima tena bila malipo, ulikuwa ni umbumbumbu wetu, lakini training ilini alert. Baad aya hapo tukaweza kwenda juu kutokana na msaada wa Media, hawa wamenisaidia sana kufanya TBS ijulikane na wananchi kuelewa umuhimu wa shirika hili kwao,” anabainisha.

Tofauti na wataalamu wengine mara wanapostaafu au hata kabla ya kufikia muda wa kustaafu hujitumbukiza kwenye siasa kwa ajili ya kutafuta umaarufu zaidi na kuacha fani zao, lakini si hivyo kwa Mwakyembe ambaye alipoulizwa iwapo ataingia kwenye siasa kwa kuwa sasa amestaafu TBS, ilimchukua nusu sekunde tu kujibu, akisema, “Hapana si yupo bwana mdogo,” anajibu bila kumtaja, lakini Mwakyembe aliyepo kwenye siasa juu kwa sasa ni Mbunge wa Kyela, Dk. Harison Mwakyembe mwenye undugu na mkurugenzi huyu mstaafu.

Mwakyembe anatoa mwito kwa uongozi wa TBS kuhakikisha hali ya kifedha inakuwa nzuri na wananchi wanaelimishwa juu ya umuhimu wa viwango katika bidhaa wanazotumia.

“Zipo bidhaa nyingi ukimuuliza mlaji atakwambia anataka nini, kwenye kutengeneza bidhaa tumuulize mlaji anataka nini, kama kukiwa na uelewa mzuri wa mlaji, bidhaa feki zisingekuwepo,” asisistiza Mwakyembe.

1 comment:

  1. tanzaniaconsumer.blogspot.com is very informative. The article is very professionally written. I enjoy reading tanzaniaconsumer.blogspot.com every day.
    instant cash loans
    payday loans canada

    ReplyDelete