Nipashe; 9 Novemba , 2007
Na Aisha Hamza, PST, Arusha
Mkazi wa Majengo mjini Arusha John Mwasapi (40) aliuza bidhaa Coco cola na Fanta ambazo ni bandia kwa kutumia nembo ya kiwanda cha Bonite Bottlers cha mjini Moshi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imeambiwa.
Akisoma shitako hilo, Mwendesha Mashitaka, Zuberi Mkakatu, alidai mbele ya Hakimu Mkama Abdallah kuwa Mwasapi alitenda kosa hilo Oktoba 20 mwaka huu, huko Mbauda.
Alizidi kudai kuwa mshitakiwa alifika katika duka la Bw. Mtega Shayo na kumuuzia mkewe kreti mbili za soda kwa bei ya Sh 5,000 kwa kreti badala ya bei ya kiwandani ya Sh 6,100 akidai kuwa alipewa na kaka yake ambaye ni mwanajeshi.
Mtuhumiwa alipoondoka mwanamke huyo aliweka vinywaji hivyo kwenye jokofu na badala ya muda mteja aliyetaka Coco cola, alikuja dukani na kupatiwa kinywaji hicho.
Alidai baada ya kunywa mteja alihisi harufu isiyompendeza inayofanana na ya ndizi na kuirudisha soda hiyo, hivyo muuzaji huyo akalazimika kumfungulia mteja huyo soda nyingine ambayo nayo ilitoa gesi kasha ikamwagika yote na mteja kubakiwa na chupa tupu.
Baada ya tukio hilo mwanamke huyo alimpigia simu mumewe na kuumweleza juu ya kuuziwa chafu lakini Bw. Shayo akamshauri kuwa anunue soda nyingine kutoka kwa Mwasapi ili iwe rahisi kumnasa.
Mwendesha Mashitaka alisema siku mbili baadaye, alirudi kuuliza kama wangehitaji soda na akaagizwa alete kreti mbili na alipozileta alikamatwa kwa kushirikiana na wananchi ambao walianza walianza kumshushia kipigo.
Mwasapi alifikishwa katika kituo kidogo cha polisi Chemchemu Mbauda na kuhojiwa kisha alipekuliwa nyumbani kwake na kukutwa na kreti tupu nyingi za soda za kampuni ya Bonite.
Pia polisi walimkamata na paketi nyingi za juisi aina ya Drink O-pop pamoja na Coke ambazo alikuwa akizitumia kutengeneza kinywaji hivyo n akuweka katika chupa hizo na kusambaza sehemu mbalimbali jijini Arusha.
Mshitakiwa alikana shitaka na kurudishwa rumande baada ya kukosa wadhamini. Kesi yake imehairishwa hadi Novemba 20.
Akizungumzia tukio hilo, mkuu wa usalama wa kituo kiwanda cha Bonite Bottlers, Bw Kundaeli Kuyata alisema, alipigiwa simu na polisi ili kwenda kukagua jinsi mtuhumiwa huyo alivyokuwa akitengeneza soda.
Alisema aligundua kuwa alikuwa anaweka unga wa juisi za Coke na Fanta kutengeneza vinywaji na unga huo ulikuwa umebaki chini ya chupa.
“Huwezi kugundua haraka ujanja wake kama si mchuuzi ndiyo maanaalikuwa anawatapeli wateja wengi. Ule unga hata ukichanganywa vipi lazima kuna chengachenga zinabaki chini ya chupa alifahamisha.
Alienda kueleza kuwa alichofanya mtuhumiwa Mwasapi ni kosa kubwa kwani alitumia nembo ya biashara ya kampuni hiyo badala ya kubuni ya kwake mwenyewe.
No comments:
Post a Comment