Nipashe ya 2007-09-13 09:55:12
Na Felix Andrew
Zaidi ya asilimia 80 ya walaji nchini, wanauelewa mdogo wa namna ya kulinda na kutetea haki zao endapo wamedhulumiwa, utafiti umebaini.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali linalotetea haki za walaji la Tanzania Consumer Advocacy Society (TCAS), Bw. Bernard Kihiyo, alisema Aprili, mwaka huu, shirika hilo lilifanya utafiti wa awali katika miji ya Arusha, Mwanza, Moshi, Pwani na Dar es Salaam.
Katika utafiti huo, jumla ya walaji 3,000 waliulizwa kuhusiana na uzoefu wao na matatizo wanayokutana nayo.
Utafiti umeonyesha kuwa, watu wanane kati ya 10 waliohojiwa, walikiri kutojua haki zao, kudanganywa na kudhulumiwa na wafanyabiashara ambao sio waadilifu, alisema.
Alisema karibu walaji wote walioulizwa hawajui ni wapi watakapopata utetezi na ushauri pindi wanapopatwa na matatizo ya udanganyifu na wizi huo.
Alidokeza kuwa, wengi wao wamekata tamaa, wakiona haki zao zikipindishwa na kuvunjwa bila utetezi ndio maana hawaoni sababu ya kujua zaidi.
``Uelewa mdogo wa walaji hao na kukosa jukwaa la kupazia sauti, umetoa mwanya kwa wafanyabiashara wenye uchu wa fedha kuendelea kutumia nafasi hiyo kuingiza bidhaa duni zisizo na ubora, pamoja na kutoa huduma zilizo chini ya viwango ukilinganisha na fedha inayolipwa na mteja,`` alisema.
Alisema kwa sasa hapa nchini kuna mapungufu makubwa ya uwajibikaji wa mashirika binafsi na yale ya kibiashara kwa jamii hususan walaji.
Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa, TCAS kama shirika wakilishi la kulinda na kutetea haki za walaji, litakuwa linatoa nafasi na uhuru kwa walaji kupaza sauti zao zisikike katika masuala yote ya kimaamuzi kuhusiana uchumi na jamii ambayo yanahusu mtiririko wa maisha yao ya kila siku.
Ili kutimiza lengo hilo alisema, TCAS ina mpango wa kuanzisha shindano la kila mwaka kushindanisha mashirika na sekta mbalimbali zinazotoa huduma bora na bidhaa zenye ubora kwa mlaji.
Alisema hiyo itaongeza changamoto kwa makampuni na wafanyabiashara kujali na kufuata haki na matakwa ya wateja kwa kanuni na miongozo iliyopo.
· SOURCE: Nipashe
No comments:
Post a Comment