Friday, July 11, 2014

Serikali yapata pigo la kwanza kodi ya simu

10th October 2013
Wanasheria Fatma Karume (kulia) na Beatus Malima wanaowakilisha Chama cha Walaji nchini wakijadiliana na mawakili wa Serikali, Alesia Mbuya (wa pili kushoto) baada ya Mahakama Kuu Kanda ya DSM
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imekubali kampuni za simu nchini kujiunga pamoja na Chama cha Kutetea Walaji kwenye kesi ya kupinga tozo ya kadi ya simu ya Sh. 1,000 kwa kila laini na mtumiaji kwa kila mwezi dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wizara ya Fedha baada ya kutupilia mbali pingamizi la awali la upande wa walalamikiwa.

Uamuzi huo ulitolewa jana na jopo la majaji watatu wakiongozwa na Mwenyekiti, Jaji  Aloysius Mujuluzi, akisaidiana na Lawrence Kaduri na Salvatory Bongole.

Jaji Mujuluzi alisema baada ya kupitia hoja zilizotolewa na pande zote mbili kuhusu pingamizi hilo, mahakama imeona upande wa walalamikiwa hauna sababu za msingi za kupinga kampuni za simu kujiunga kwenye kesi hiyo na kwamba inazitupilia mbali.

Aidha, baada ya uamuzi huo mahakama iliziamuru pande zote mbili kubadilishana nyaraka za majibishano ya kisheria kwa njia ya maandishi na kesi ya msingi itasikilizwa Oktoba 21, mwaka.

Kampuni zilizojiunga kwenye kesi hiyo ni, Vodacom, Airtel, Mic Tanzania Ltd, TTCL na Zantel Tanzania. Jumatatu iliyopita, upande wa walalamikiwa ukiongozwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, akisaidiana na Wakili wa Serikali Mkuu, Edson Mweyunge, Alisia Mbuya na Sara Mwaipopo, walipinga ombi la mawakili wa kampuni za simu la kutaka kujiunga kwenye kesi hiyo kwa kuwa hati ya kiapo ilikosewa kisheria.

Mweyunge alidai kuwa hati ya kiapo iliyowasilishwa mahakamani  imeonyesha kutolewa na Tumaini Shija ambaye anawawakilisha walalamikiwa wengine zikiwamo makampuni za simu.

Hata hivyo, wakili wa kampuni  za simu, Fatuma Karume, alidai kuwa pingamizi la jamhuri halina sababu za msingi kwa sababu siyo kila mlalamikaji anatakiwa kuwasilisha kiapo chake  katika kesi moja kwamba mahakama itupilie mbali pingamizi la jamhuri halina msingi kisheria.

Katika kesi ya msingi Chama cha Kutetea Walaji kimewaburuza mahakamani Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wizara ya Fedha kikitaka wapewe amri ya kusimamisha tozo ya kadi ya simu ya Sh. 1,000 kwa kila laini kwa watumiaji wa simu kila mwezi, baada ya kupitishwa na Bunge miezi michache iliyopita.
SOURCE: NIPASHE

No comments:

Post a Comment