Sunday, March 16, 2008

Uingizaji bidhaa bandia nchini tishio kwa watumiaji

Nipashe 14-03-200
Na Felix Andrew

Kutokana na kuongezeka kwa bidhaa zisizo kidhi ubora nchini na sehemu nyingine serikali kwa kushirikiana na wadau kadhaa wamekuwa makini katika kuhakikisha kuwa afya za walaji zinalindwa na kusimamiwa ipasavyo.

Sio siri, baada ya uamuzi wa kuwa na soko huria, Tanzania inakabiliwa na changamoto ya uingizaji wa bidhaa za aina mbali mbali ambazo nyingi hazikidhi viwango, jambo linalohatarisha afya za walaji. Lakini pia inatia moyo kuona kuwa serikali inaonyesha kuwa ipo makini katika kukabiliana na hilo ili kulinda afya za watu wake.

Serikali imekuwa ikisema katika mfumo wa kujenga uchumi wa soko, majukumu yake ya msingi ni kuweka mazingira bora, kuhakikisha kwamba unakuwepo ushindani wa haki baina ya washiriki wa ndani na kati ya washiriki wa ndani na wa nje na wakati huo huo, kuhakikisha kwamba maslahi na afya za walaji hazidhuriki kutokana na uhafifu wa bidhaa zinazozalishwa ndani au kuingizwa kutoka nje.

Aidha, watumiaji wa huduma na bidhaa zinazozalishwa au kuingizwa katika soko kutoka nje, wanahitaji kulindwa kutokana na kutozwa bei au gharama za juu sana. Kwa mtazamo huo, uanzishwaji wa Tume ya Ushindani (Fair Competition Commission) pamoja na Mamlaka za Udhibiti una lengo la kuboresha ushindani, kuboresha ubora wa viwango vya bidhaa na huduma na kulinda walaji.

Taasisi zilizoundwa kwa lengo la kulinda afya za walaji ni pamoja na Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, National Food Control Commission na taasisi ya kudhibiti ubora wa bidhaa Tanzania. Pamoja na kuunda mamlaka na taasisi hizo kwa lengo la kuimarisha ushindani wa haki na kulinda mlaji, Serikali vile vile inaendeleza mipango ya kuimarisha maabara za uchunguzi wa kemikali na vimelea haribifu itakayokidhi viwango vya Kimataifa kama ule unaojengwa huko Mwanza kwa ajili ya biashara ya minofu ya samaki.

Ni matumaini ya Serikali kwamba baada ya kuweka mazingira bora ya ushindani pamoja na kumlinda mlaji, uchumi wa soko utaendeshwa kwa mfumo na utaratibu ulio bora zaidi na unaojali afya na maslahi ya mlaji kwa ujumla. Katika jitihada za kulinda haki za walaji, taasisi binafsi zimekuwa mstari wa mbele ili kuhakikisha kuwa walaji wanajiepusha na tabia ya matumizi ya vitu vilivyo chini ya viwango.

Hivi sasa sehemu mbalimbali duniani, ikiwemo Tanzania wamekuwa katika maandalizi ya kusherekea siku ya haki za walaji duniani itakayoadhimishwa katikati ya mwezi huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kutetea Haki za walaji Tanzania (TCAS) Bw Bernard Kihiyo, anasema kuwa maadhimisho hayo yanayotarajia kufanyika Machi 15 yanalenga kuikumbusha jamii vitendo vya ukiukwaji wa haki za walaji duniani.

Mwaka huu ujumbe wa siku hiyo unasema zuia kutangaza vyakula vibovu. Vyakula vibovu ni pamoja na vile vyenye sukari, chumvi na mafuta na havionyeshi vizuri muda wake wa kumalizika lakini vinafanyiwa matangazo ya hali ya juu kuwa bado vinafaa kwa matumizi ya binadamu, inakuwa ni ngumu sana kusema chakula au kinywaji gani ni kizuri au siyo kizuri kwa afya.

Anasema kuwa TCAS imedhamiria kuandaa wiki ya walaji ambapo mambo mbali mbali yatakuwa yanafanyika kabla ya kufika kilele cha sherehe. Katika wiki hiyo anasema chama kitaandaa mkutano kuhamasisha wananchi na taasisi mbali mbali juu ya siku hiyo.

Taasisi zinazotarajiwa kualikwa kwenye mkutano huo ni madaktari , Shirika la Viwango nchini (TBS) na Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA). Pia alisema siku ya kilele, TCAS itaandaa maandamano ya amani kutoka Kariakoo hadi Viwanja vya Mnazi mmoja ambapo viongozi mbali mbali watatoa hotuba zao.

Siku ya haki za walaji duniani ilianza kuadhimishwa nchini Marekani ambapo mnamo Machi 15 mwaka 1962 Rais John. F Kennedy alitoa tangazo kwa baraza la Congress. Anasema walaji ndilo kundi kubwa kabisa la kiuchumi lililoathirika au kuathiriwa na maamuzi mengi ya umma na pia ndio kundi muhimu ambalo mawazo yake mengi hayasisiki.

Katika mkutano huo Rais Kennedy alitangaza haki nne za msingi za walaji ambazo wananchi wa Marekani wanazitambua hadi leo.Haki hizo ni haki ya usalama, haki ya kupewa taarifa, haki ya kuchagua na haki ya kusikilizwa. Kwa mara ya kwanza Siku ya Walaji Duniani ilianza kuadhimishwa Machi 15 mwaka 1983 nchini Marekani , Uingereza na baadaye katika nchi nyingine kama Misri, Kenya, Zimbabwe, Nigeria, Ghana, Afrika Kusini na imekuwa ikihamasishwa kwa kushirikiana na taasisi ya kimataifa ya kutetea haki za walaji inayojulikana na Consumers International (CI).

Utafiti uliofanywa na TCAS mwezi Aprili mwaka jana katika miji ya Arusha, Mwanza, Moshi, Pwani na Dar es Salaam unaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya walaji nchini hawana uelewa wa kutosha kuhusiana na haki zao.

Kutokana na uelewa finyu wa mlaji kuhusiana na sheria , wafanyabiashara ambao sio waadilifu wameendelea kutumia mwanya huu kudanganywa na kudhulumu walaji kwa kuleta bidhaa duni na zisizokidhi malengo ya watumiaji yaani walaji.

Wakizungumza katika mahojiano, wananchi wengi wanasema kuwa bado hawajazijua haki za mlaji, na hivyo wameomba kuelimishwa zaidi kuhusiana nazo. ``Kwa kweli mimi binafsi bado sijajua nifanye pindi ninapogundua kuwa bidhaa niliyouziwa ni feki au mahali pa kulalamika, `` anasema Bi Rozina Mwambe mkazi wa Kijitonyama.

Mwananchi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Jerome Sanga,anakiri kuwa bado hajajua haki hizo na kuziomba taasisi husika kutoa elimu kwa wananchi namna ya kuzijua na kuzidai. ``Nimekuwa nikiwaona watu wa tume ya ushindani wakikamata na kuziteketeza bidhaa feki, lakini bado sijawahi kusikia wananchi walionunua bidhaa hizo kwa bahati mbaya kama wanapewa fidia au la``, amesema. Hivi karibuni Bunge la Jamhuri ya Muungano lilipitisha sheria kali zaidi ya kudhibiti bidhaa Bandia ambapo kundi kubwa zaidi la watu linalojihusisha na bidhaa hizo litaweza kubanwa ikiwa ni pamoja na wauzaji reja reja na hatua hiyo kuchukua muda mfupi.

Sheria hiyo kwa sasa inasubiri saini ya Rais ili iweza kuanza kutumika rasmi. Mashirika ya kupigania haki za walaji hayana budi kuendelea kuelimisha walaji kuhusiana na haki zao ili kupunguza wigo wa tatizo la dhuluma na uonevu kutoka kwa wafanyabiashara wafanyabiashara wasio waadilifu.

Kwa mujibu wa sheria ya ushindani ya mwaka 2003, imeainisha mambo yote ambayo ni kinyume na taratibu za kibiashara, na imebainisha ni mambo gani yakikiukwa mlaji au mdau mwingine yeyote ana haki ya kushtaki na kulipwa fidia pale ikibainika kuwa ameathirika na tukio la ukiukwaji wa vipengele tajwa, sehemu ya nne, kipengele cha 22 hadi 24 imebainisha hiyo na pia sehemu ya kumi kipengele cha 57 mpaka 91 kimeainisha Mahakama ya ushindani ikiwa ni pamoja na taratibu, mamlaka na majukumu ya Mahakama hii kwa wabia wa biashara ikiwa ni pamoja na mlaji.

Pamoja na kuanzisha sheria mbalimbali za kumlinda mlaji, utafiti unaonyesha kuwa hadi leo hii bado Tanzania inakabiliwa ukiukwaji mkubwa wa haki za walaji kupitia serikali na mawakala wake, wazalishaji, waagizaji wa bidhaa na pia kutoka katika makundi mengine ya jamii yenye nguvu, huku mlaji hajui ni kwa vipi ataweza kukabiliana na kadhia hii.

Kutokana na hili imeonekana ni muhimu kubainisha haki za mlaji katika jitihada za kuwasaidia walaji kuelewa haki zao za msingi ili mlaji aweze kupaza sauti yake kupitia jukwaa la TCAS.

Serikali na wadau wanatakiwa kuanza kuwashirikisha walaji ili wazielewe haki zao na namna ya kuzifuatilia ,kinyume na hapo itakuwa vigumu sana kupambana na uingizaji wa bidhaa feki nchini. Sheria iliyoanzisha TBS inayoipa mamlaka ya kuujulisha umma juu ya bidhaa zisizokuwa na viwango haina budi kuangaliwa upya.

Chini ya sheria hiyo, wakati mwingine TBS hulazimika kuiomba Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati (Ewura) kutumia sheria yake, kuwachukulia hatua watu waliokiuka sheria. Inatakiwa TBS ipewe meno yenye `kuuma` pindi panapotokea uvunjaji wa sheria tulizojiwekea badala ya kuzikabidhi taasisi nyingine.

SOURCE: Nipashe Fuatilia link hii

www.ippmedia.com/ipp/nipashe/2008/03/14/110327.html

No comments:

Post a Comment