Sunday, December 2, 2007

Bidhaa feki: wananchi waelimishwe wazikatae

Nipashe; 2007-09-21 09:03:16

Na FELIX ANDREW

Tatizo la bidhaa feki huenda likapungua iwapo wananchi wataelimishwa kuhusu haki zao, madhara ya bidhaa hizo, na serikali kuweka ulinzi wa kutosha kuzuia uingizaji wake.

Tangu kuruhusu soko huria mnamo miaka ya 80 nchi yetu imejikuta katika matatizo makubwa sana ambayo endapo hayatashughulikiwa yanaweza kulipeleka pabaya taifa ,kiuchumi, kiafya na kiutamaduni.

Moja ya tatizo kubwa linalotokana na mfumo wa soko huria ni uingizaji wa bidhaa feki ambao umekuwa unaongezeka kila siku.

Kwa sasa Tanzania imegeuka kuwa soko la bidhaa hizo, kwa kutokujua wananchi wameendelea kununua bidhaa hizo ambazo zina kiwango cha chini, na nyingine zina athari kwa afya zao.

Baada ya kelele kutoka kwa wadau mbalimbali serikali imeamka, na kuanza kuchukua hatua kadhaa ili kuondokana na tatizo hilo

Akizungumza na waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Basil Mramba, alisema tayari serikali kwa kupitia idara zake mbalimbali imeanza kukamata bidhaa `feki` zinazoingizwa nchini toka nje, zikiwemo dawa na vyakula.

Amewataka wananchi kutokimbilia bidhaa za nje ambazo bei zake ni rahisi, kwani hazina ubora unaotakiwa na ni hatari kwa afya zao.

Alisema kwa kawaida bidhaa hizo, hazionyeshi mtengenezaji ni nani, mbali na kuwa na maandishi ya kujisifu.

`Ninawatahadharisha wananchi wanaponunua bidhaa mbalimbali wawe waangalifu, wasivutiwe na bei nzuri tu, lakini wajue wanaumizwa, wanalanguliwa, wanatapeliwa na wanaziweka rehani afya zao,`alisema waziri Mramba.

Bw. Mramba alisema, bidhaa feki ni hatari kwa maisha na uchumi wa nchi kwa kuwa zinaharibu soko la bidhaa za ndani.

Alitoa mfano, kuwa tairi feki za magari zinaweza kusababisha ajali kwa kuwa zinapasuka muda wo wote wakati gari ikiwa barabarani.

Baadhi ya bidhaa feki zinazolalamikiwa ni pamoja na dawa za meno, vifaa vya umeme, vyakula na matairi ya magari.

Mbali na tatizo la bidhaa feki, pia inaonekana kuwa wananchi wengi (walaji) bado wana uelewa mdogo sana wa kulinda na kutetea haki zao pindi wanapodhulumiwa .

Mathalani ni mara ngapi tumesikia walaji wakilalamika kuuziwa chakula kibovu? au kufidiwa kutokana na madhara yanayotokana na kutumia chakula hicho?.

Utafiti unaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya walaji nchini hawana uelewa wa kutosha kuhusiana na haki zao.

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali linalotetea haki za walaji linalojulikana kama Tanzania Consumer Advocacy Society (TCAS) Bw. Bernard Kihiyo ,anasema mapema mwezi Aprili mwaka huu shirika hilo lilifanya utafiti wa awali katika miji ya Arusha, Mwanza, Moshi na Dar es Salaam.

Utafiti huo, ulishirikisha jumla ya walaji 3,000 walioulizwa kuhusiana na uzoefu wao na matatizo wanayokutana nayo.

Utafiti umeonyesha kuwa watu wanane kati ya kumi waliohojiwa wamekiri kutojua haki zao, kudanganywa na kudhulumiwa na wafanyabiashara ambao sio waadilifu, alisema.

Anasema karibu walaji wote walioulizwa hawajui ni wapi watakapopata utetezi na ushauri pindi wanapopatwa na matatizo ya udanganyifu na wizi huo.

Alidokeza kuwa wengi wao wamekata tamaa, wakiona haki zao zikipindishwa na kuvunjwa bila utetezi ndio maana hawaoni sababu ya kujua zaidi.

`Uelewa mdogo wa walaji hao na kukosa jukwaa la kupazia sauti,umetoa mwanya kwa wafanyabiasha wenye uchu wa fedha kuendelea kutumia nafasi hiyo kuingiza bidhaa duni zisizo na ubora, pamoja na kutoa huduma zilizo chini ya viwango ukilinganisha na fedha inayolipwa na mteja`,alisema.

Alibainisha kuwa kwa sasa hapa nchini kuna mapungufu makubwa sana ya uwajibikaji wa mashirika binafsi na yale ya kibiashara kwa jamii hususan walaji.

Bw Kihiyo aliongeza kuwa, TCAS kama shirika wakilishi la kulinda na kutetea haki za walaji, litakuwa linatoa nafasi na uhuru kwa walaji kupaza sauti zao zisikike katika masuala yote ya kimaamuzi kuhusiana na uchumi na jamii ambayo yanahusu mtiririko wa maisha yao ya kila siku.

Ili kutimiza lengo hilo alisema, TCAS ina mpango wa kuanzisha shindano la kila mwaka kushindanisha mashirika na sekta mbalimbali zinazotoa huduma bora na bidhaa zenye ubora kwa mlaji. Hii itaongeza changamoto kwa makampuni na wafanyabiashara kujali na kufuata haki na matakwa ya wateja kwa kanuni na miongozo iliyopo.

Bw. Kihiyo alisema, TCAS ingependa kuona kwamba wafanyabiashara wa umma na binafsi wote wanakuwa na lengo moja la kufuata na kutekeleza miongozo ya biashara ya haki ambayo inalenga kumsaidia mlaji.

Katika kuimarisha huduma kwa walaji nchini, Mkurugenzi huyo alisema shirika hilo lenye makao yake Barabara ya Morogoro eneo la Mbezi pia lina mpango wa kuanzisha vikundi mbalimbali vya walaji ili waweze kujiunga pamoja kuzungumza na kutetea haki zao, pia zitakuwepo huduma za kuzunguka vijijini na mijini kuelimisha na kuelezea haki na wajibu wa mlaji katika mazingira ya soko huria.

Kwa upande mwingine Shirikisho la Wenye Viwanda Nchini (CTI) limesema serikali inatakiwa kuchukua hatua za haraka ili kudhibiti bidhaa feki katika soko la ndani.

Limeishauri serikali kutoa elimu kwa wadau wote juu ya hatari inayoweza kutokea kutokana na bidhaa feki kwa lengo la kuzizuia katika soko. Watalaam wa masuala ya afya wanaonya wananchi kuwa makini pindi wanaponunua bidhaa mbalimbali ikiwemo vyakula kutoka kwenye maduka.

Wanasema kuwa vingi ya vyakula hivyo vimepita muda wake wa matumizi na huenda vinaweza kuwaletea matatizo

Baadhi ya bidhaa ambazo mathalani zilionyesha muda wake wa kumaliza kutumika kuwa ni Februari 14, mwaka huu bado ziliendelea kuwepo katika maduka hayo, anasema Bw. Ngonela Mwandambo.

Wafanyabiashara wengi wamekuwa wakiuza bidhaa hizi waziwazi kwa visingizio kwamba iwapo hawatafanya hivyo wataingia hasara!

Kwa upande mwingine, hata zile mamlaka zinazohusika na uhakiki wa ubora wa bidhaa kama vile Taasisi ya Viwango Tanzania (TBS), Idara za Biashara kwenye manispaa mbalimbali na Wizara ya Afya nazo zimekuwa hazifuatilii vya kutosha kuhakikisha kwamba tatizo hili linadhibitiwa.

Majukumu ya msingi ya Serikali ni kuweka mazingira bora, kuhakikisha kwamba unakuwepo ushindani wa haki baina ya washiriki wa ndani na kati ya washiriki wa ndani na wa nje na wakati huo huo, kuhakikisha kwamba maslahi na afya za walaji hazidhuriki kutokana na uhafifu wa bidhaa zinazozalishwa ndani au kuingizwa kutoka nje.

Aidha, watumiaji wa huduma na bidhaa zinazozalishwa au kuingizwa katika soko kutoka nje, wanahitaji kulindwa kutokana na kutozwa bei au gharama za juu sana.

Kutokana na umuhimu wa kuwa na ushindani wa haki pamoja na kulinda walaji ndiyo maana Serikali katika nyakati mbalimbali imekuwa ikiunda taasisi za kudhibiti ushindani na kusimamia ubora wa bidhaa na huduma kwa lengo la kulinda wala ji.

Taasisi zilizoundwa kwa lengo la kulinda afya za walaji ni pamoja na Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, National Food Control Commission na taasisi ya kudhibiti ubora wa bidhaa Tanzania.

Mamlaka ya Kudhitibi Sekta ya Nishati na Maji, Mamlaka ya Kudhibiti Usafiri wa nchi kavu na majini, Mamlaka ya kudhibiti usafiri wa anga, Kamisheni ya kudhibiti upashanaji habari na matangazo, Mahakama ya mwenendo wa haki katika biashara na Mamlaka ya kudhibiti mawasiliano.

Kinachotakiwa ni viwanda vijitahidi kuzalisha kwa gharama ndogo ili nao wauze kwa gharama ndogo na walaji waweze kupata bidhaa zao.

Ni wazi kabisa ikiwa bidhaa zitakuwa bora na bei itakuwa ya chini basi wananchi wengi au walaji wengi watakimbilia kununua bidhaa za ndani kuliko kukimbilia kununua bidhaa za nje.
· SOURCE: Nipashe

No comments:

Post a Comment